Mbona Basi Mnaifanya Migumu Mioyo Yenu?
“Mbona, basi mnaifanya migumu mioyo yenu, kama vile
wale Wamisri, naye yule Farao, walivyoifanya mioyo yao?...” 1Samweli 6:6
Bwana Yesu Kristo asifiwe!
Ni jambo jema kumshukuru Mungu kwa kutupa kibali
tena cha kuiona siku hii nyingine na wiki nyingine tena ya leo. Namshukuru mungu
kwa wema na fadhili zake zinazotufuata siku zote za maisha yetu kila iitwapo
leo.
Leo ningependa kuongea na wewe ambaye umekuwa unafanya
moyo wako kuwa mgumu na hutaki kuisikia sauti ya Mungu na kumpa Yesu maisha
yako. Naongea pia na wewe ambaye umeanguka dhambini na umeshindwa kurudi kwa
Yesu tena.
Mbona unaufanya moyo wako kuwa mgumu? Mbona utaki
kuokoka? Nini kinakuzuia kumpa Yesu maisha yako? Je ni mali au shughuli za
dunia? Je ni wazazi, ndugu au mpenzi? Je unajiona bado wewe ni mdogo na unasema
ngoja nile ujana kwanza, Yesu badae? Je dhambi zimekuzidia unaona kwamba huwezi
kuziacha? Sijui sababu yako ni ipi ndugu yangu inayokufanya usimpe Yesu maisha
yako.
Wakati ni sasa wa kumpokea Yesu na wala hakuna
wakati mwingine, usiseme kesho kwa sababu hakuna aliye na uwakika na kesho.
Nisikilize ndugu yangu Yesu anakupenda sana. Laiti
ungejua usingefanya moyo wako kuwa mgumu kabisa. Alikufa pale msalabani kwa
ajili ya dhambi zako. Aliteseka kwa ajili yako. Upendo wake kwako hauna kipimo.
Ni upendo ambao kwa akili za kibinadamu huwezi kuelezea.
“Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata
akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa
milele.” Yohana 3:16
Usiache upendo huu ambao Yesu anao kwako kukupita
bure. Usikubali kuendelea kuteseka na dhambi, wakati yupo ambaye amekufa ili
wewe upone.
Wewe ambaye umeanguka kwenye dhambi, mbona unaufanya
moyo wako kuwa mgumu? Unasuburi nini kurudi tena kwa Yesu? Hata kama umeanguka
zaidi ya mara moja, Yesu yupo tayari kukupokea tena. Tubu na urudi kwake. Nje uko
kuna mbwa mwitu wakali, rudi kunduni mwa kondoo, usikubali kuendelea kuwa
mtumwa wa hiyo dhambi?
Mungu anabisha kwenye mlango wa moyo wako anataka
kukuokoa, anataka kukusaidia, anataka kukuponya, anataka kukupa uzima wa
milele, anataka kukutoa kwenye utumwa wa dhambi, anataka kukupa amani na furaha
ya kweli. Je uko tayari kumpokea?
“Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia
sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye,
na yeye pamoja nami.” Ufunuo wa Yonana
3:20
UFALME WA MUNGU UMEKARIBIA. USISEME KESHO KWA SABABU
KESHO HUJUI UTAKUWA WAPI. WAKATI NI SASA. YESU ANAKUPENDA. MPOKEE YESU LEO
ABADIRISHE MAISHA YAKO.

Maoni