Wewe Ni Raia Wa Mbinguni
Yohana 17:14-16
[14]Mimi nimewapa neno lako; na ulimwengu umewachukia; kwa kuwa wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu.
[15]Mimi siombi kwamba uwatoe katika ulimwengu; bali uwalinde na yule mwovu.
[16]Wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu.
Bwana Yesu Mfalme asifiwe!
Nazidi kumshukuru Mungu kwa wema na fadhili zake kwenye maisha yetu ambazo hazikomi kila kukicha. Kila asubuhi fadhili za Mungu ni mpya kwetu. Ni jambo jema na la kupendeza kumshukuru Mungu kwa jinsi ambavyo anatupigania, kutulinda na kuturehemu kila siku na kila muda.
Leo natumia nafasi hii kukukumbusha kwamba wewe ambaye umempa Yesu maisha yako, ni raia wa Mbinguni. Maneno tuliyosoma kwenye kitabu cha Yohana 17 hapo juu ni miongoni mwa maombi amabayo aliyafanya Bwana Yesu kabla ya kwenda msalabani. Ni maombi ambayo ndani yake yanatukumbusha kwamba sisi sio raia wa dunia, bali uraia wetu ni wa Mbinguni.
Ukisoma mlango wa 17 wa kitabu cha Yohana utaona jinsi ambavyo Bwana Yesu alituombea kwa Baba ulinzi kwa sababu sisi ni raia wa Mbinguni ( soma Yohana 17:11). Lakini pia alisema ulimwengu huu unatuchukia kwa sababu sisi sio wa ulimwengu huu (Soma Yohana 17: 14). Tena mstari wa 15 na 16 anamuomba Mungu Baba atulinde zidi ya yule muovu yaani shetani kwa sababu sisi sio wa ulimwengu kama Yeye Yesu asivyo wa ulimwengu huu.
Baada ya kuokoka mwana wa Mungu unaamishwa kutoka kwenye ufalme wa giza na kuingizwa kwenye Ufalme wa Mungu. Soma maneno haya: Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake; (Wakolosai 1:13). Kama hujazaliwa mara pili maana yake unaishi kwenye Ufalme wa giza na baada ya kuzaliwa mara ya pili unaingizwa kwenye Ufalme wa Mungu.
Kwa hiyo unapookoka unakuwa mwana wa Ufalme wa Mungu na unaingizwa kwenye Ufalme wa Mungu na kuhesabika kama raia wa Mbinguni moja kwa moja.
Wewe amabaye umeokoka kumbuka wewe ni raia wa Mbinguni mpendwa. Maisha yako na tabia zako zinatakiwa zioneshe na kuakisi maisha ya Ufalme wa Mungu.
Ingawa unaishi duniani lakini kumbuka duniani sio kwako, makao yako makuu au Headquarter za Ufalme wako ni Mbinguni. Upo Duniani kuwakilisha Ufalme wa Mungu. Wewe ni balozi wa Ufalme wa Mungu duniani.
Usisahau hata siku moja kwamba wewe ni raia wa Mbinguni. Kuzaliwa mara ya pili ndio njia ya wewe kuingia kwenye Ufalme wa Mungu (Soma Yohana 3:3)
Ishi kama mtoto wa Ufalme wa Mbinguni. Nenda kama mtoto wa Ufalme wa Mbinguni.
Nikomee hapa kwa leo. Baraka na wema wa BWANA Yesu viwe pamoja nawe. Amen.
WEWE AMBAYE HUJAMPA YESU MAISHA YAKO, UNASUBIRI NINI. WAKATI NI SASA, SIO KESHO, KWA SABABU HUJUI NINI KITATOKEO KESHO. MPE YESU MAISHA YAKO. ZALIWA MARA YA PILI NA UINGIE KATIKA UFALME WA MUNGU. YESU ANAKUPENDA NA ALIKUFA PALE MSALABANI KWA AJILI YAKO. USIACHE NEEMA HII IKUPITE LEO. HAKUNA TIKETI NYINGINE YA KUINGIA KWENYE UFALME WA MUNGU ZAIDI YA KUMKUBALI YESU KUWA BWANA NA MWOKOZI WA MAISHA YAKO. MPE NAFASI KWENYE MAISHA YAKO LEO NA HUTAJUTA.
Maoni