Endelea Mbele (Bwana Atakupigania, Nawe Utanyamaza Kimya)

“Musa akawaambia watu, Msiogope, simameni tu, mkauone wokovu wa BWANA atakaowafanyia leo; kwa maana hao Wamisri mliowaona leo hamtawaona tena milele. BWANA ATAWAPIGANIA NINYI, NANYI MTANYAMAZA KIMYA. BWANA akamwambia Musa, Mbona unanililia mimi? WAAMBIE WANA WA ISRAELI WAENDELEE MBELE.” Kutoka 14: 13-15



Bwana Yesu Kristo asifiwe milele!

Namshukuru Mungu sana kwa kutupa neema ya kumtumikia siku nyingine nzuri ya leo. Rehema na fadhili zake ni nyingi mno katika maisha yetu. Ni rehema zake tu kwamba hatuangamii na fadhili zake ni mpya kila siku asubuhi.

Leo nimetumwa kukuhamasisha wewe ambaye unapita katika kipindi kigumu kwenye maisha yako. Wewe ambaye mbele yako unaona bahari ya shamu na akili zako zimefika mwisho na huoni mpenyo wa kutokea hapo unapopita. Nimetumwa leo nikutie moyo na kukukumbusha kuwa Mungu amehaidi atakupigania nawe utanyamaza kimya.

Wana wa Israeli walifika sehemu wakapata hofu kuu pale ambapo walikutana na bahari ya shamu mbele yao na nyuma yao kulikuwa na jeshi kubwa na la kutisha la Wamisri. Walifika sehemu wakakata tamaa kabisa na kuona huo ndio mwisho wao na hakuna tena tumaini mbele yao.

Lakini tunamuona mtumishi wa Mungu, Musa akiwatia moyo na kuwaambia wasiogope, wasimame tu, wakauone wokovu wa Bwana atakaofanya; kwa maana hao Wamisri mliowaona leo hamtawaona tena milele. Bwana atawapigania ninyi, nanyi mtanyamaza kimya.

Wewe ambaye unapita mahali pagumu sikia Neno la Bwana; USIOGOPE, SIMAMA KIUME TU, UKAUONE WOKOVU WA BWANA ATAKAOFANYA; KWA MAANA HAO WAMISRI( MAHALI PAGUMU UNAPOPITIA, ILO JARIBU, HIYO SHIDA, HIYO HOFU KUU)  HAUTAIONA TENA MILELE. BWANA ATAKUPIGANIA WEWE, NAWE UTANYAMAZA KIMYA.

Mungu anakwambia endelea mbele tu, endelea mbele, usikate tamaa. Ndio anajua mbele yako kuna bahari ya shamu, ndio anajua mbele yako kuna jaribu. Unapoona huoni mwisho wake na inawezekana umekaa hapo muda mrefu na umeshindwa kutoka. Akili zimegoma, hakuna anayekupa msaada, marafiki na ndugu wamekukimbia. Lakini Bwana anasema ENDELEA MBELE, USIKATE TAMAA, NITAIPASUA HIYO BAHARI YA SHAMU NA WEWE UTAPITA SALAMA.

Mungu anataka uchukue hatua ya imani ya kuendelea mbele bila woga wala hofu, ukimwamini kwamba hiyo bahari sio kitu kinachomshinda Yeye. Anaweza akakupitisha kwenye hiyo bahari kama tu utamwamini Yeye.

Mungu amehaidi atafanya mlango wa kutokea kwenye ilo jaribu. Mwamini Mungu na uendelee mbele, usikate tamaa, Yeye amehaidi kukutetea na kukusadia. USIRUDI NYUMA, ENDELEA MBELE KWA IMANI.

“Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu; ila Mungu ni mwaminifu; amabye hatwaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu ATAFANYA NA MLANGO WA KUTOKEA, ili mweze kustahimili.” 1 Wakorintho 10:13

“Usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako; NITAKUTIA NGUVU, NAAM, NITAKUSAIDIA, naam, nitakushika kwa mkono wa kuume wa haki yangu.” Isaya 41:10

Nikomee hapa kwa leo. Baraka na wema wa Bwana viwe pamoja nawe sasa na hata milele. AMEN.

YESU ANAKUPENDA WEWE AMBAYE HUJAMPA MAISHA YAKO. UFALME WA MUNGU UMEKARIBIA SANA. UNASUBIRI NINI KUMPOKEA YESU NA KUMTUMIKIA? WAKATI NI  SASA. MPOKEE YESU AWE BWANA NA MWOKOZI WA MAISHA YAKO LEO.

“Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.” Yohana 3:16
Usikubali kupotea kwa kutokumwamani Yesu. Fanya maamuzi muhimu leo ya kumpokea Yesu, kwa sababu YESU NI NJIA, KWELI NA UZIMA (Yohana 14:6)


Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Maamuzi Magumu (Wakoma Kishindo Cha Jeshi Kubwa)

Wewe Ni Raia Wa Mbinguni