Maamuzi Magumu (Wakoma Kishindo Cha Jeshi Kubwa)
“Basi walikuwako watu wanne wenye ukoma, penye lango
la mji; wakasemezana, Mbona tunakaa hapa hata tufe? Tukisema, tutaingia mjini,
mjini mna njaa, nasi tutakufa humo; nasi tukikaa hapa, tutakufa vile vile.
Haya! Twende tukaliendee jeshi la Washami; wakituhifadhi hai tutaishi;
wakituua, tutakufa tu.” 2Wafalme 7: 3-4
Bwana Yesu asifiwe!
Namshukuru Mungu kipekee kabisa kwa kutupa neema ya
kuiona siku hii mpya ya leo. Ni huruma zake tu kwamba hatuangamii. Fadhili zake
ni mpya kila inapoitwa leo.
Leo Mungu ametupa tujifunze kuchukua maamuzi magumu.
Maamuzi magumu waliyoyachukua wakoma hawa yaliwaokoa wao na Israeli yote kutoka
kwenye njaa kali. Kama hawa wakoma wasingefanya maamuzi magumu kwa kuangalia
hali walizonazo sijui kama chakula kingepatikana.
Walichukua maamuzi ambayo yalihatarisha maisha yao.
Walikuwa tayari kupoteza maisha yao kwa sababu walijua hata kama wangebaki pale
walipo wangekufa tu. Walichukua maamuzi ya kufa na kupona na kupitia maamuzi
yao Israeli yote ilipona kutoka kwenye njaa kali.
Na kwa kuwa walikuwa tayari kuthubutu na kuchukua
maamuzi magumu, Mungu alitumia miguu yao na kuzifanya ziwe kishindo cha jesi
kubwa na washami wakapata hofu kuu na kukimbia na kuacha vitu vingi vikiwemo
vyakula na mali kwenye kambi yao.
Tunajifunza nini kutokana na maamuzi magumu
waliyochukua wakoma hawa wanne?
Mungu hahitaji mtu mwenye nguvu nyingi au akili
nyingi au mtu maarufu ili afanye kazi yake. Mungu anahitaji mtu ambaye atasema
mimi hapa Bwana nitumie. Haijalishi uwezo wake alionao. Anahitaji mtu anayeweza
kufanya maamuzi magumu bila kuangalia hali alizonazo.
Mungu aliwatumia wenye ukoma kufukuza jeshi la
washami. Mungu anaweza kukutumia wewe kufanya mambo makubwa bila kujali au
kuangalia udhaifu wako. Anachohitaji ni wewe kufanya maamuzi magumu bila
kuangalia hali uliyonayo.
Hawa watu wanne wangeweza kusema sisi hatuwezi bana
tuna ukoma, tukae tu hapa tufe hamna haja ya kujisumbua. Lakini walichukua
maamuzi magumua bila kuangalia hali waliyonayo na kupitia kwao waliliokoa taifa
zima la Israeli.
Inawezekana unasema hali ni mbaya siwezi kufanya
maamuzi. Kuna vitu ukiviona kwenye maisha yako unaona kama vinakuwa sababu ya
wewe kutokuchukua maamuzi. Kumbuka hali uliyonayo sio sababu ya wewe
kutokuchukua maamuzi.
Nani amekwambia Mungu anataka mtu aliyekamilika?
Nani amekwambia Mungu anataka mtu mwenye hekima au akili nyingi? Nani
amekwambia? Unachelewa kuchukua hatua leo ya kufanya jambo hilo kwa sababu
unaona udhaifu ulionao.
Familia yako inawezekana inapitia kipindi kigumu kwa
sababu ya wewe kutokuchukua maamuzi magumu. Inawezaekana hata taifa linapitia
kipindi fulani kigumu kwa sababu tu kuna watu wachache walitega kusimama kwenye
nafasi zao na kuchukua maamuzi magumu kwenye mambo fulani.
Ni bora ukachukua hatua leo hata kama utakosea
kuliko kuendelea kukaa hapo tu bila kufanya kitu chochote. Kama wakoma
wangeendelae kukaa pale hakika wangekufa na unajua hata taifa la Israeli
lingeendelea kubaki na njaa kali na watu wengi wangekufa. Mungu ashukuriwe
kwamba hawa jamaa walikuwa tayari kufanya maamuzi ya kufa na kupona na kwa
sababu hiyo wakapona wao na taifa lao.
“Basi wakaondoka kabla ya mapambazuko, ili waende
mpaka kituo cha Washami; walipofika mwanzo wa kimo cha Washami, kumbe! Hapana
watu. Kwa maana Bwana alikuwa amewasikizisha Washami KISHINDO CHA FARASI, KAMA
KISHINDO CHA JESHI KUBWA; wakaambiana, Tazama, mfalme wa Israeli amewaajiri
wafalme wa Wahiti, na wafalme wa Wamsiri, waje wapigane nasi.” 2 Wafalme 7: 5-6
Wewe ni kishindo cha jeshi kubwa. Unaweza kufanya
makubwa kama utaamua kuchukua hatua leo. Wale wakoma inawezekana wangejidharau
na kusema sisi hatuwezi, lakini walipoamua, Mungu aliwatumia kama kishindo cha
jeshi kubwa.
Nikomee hapa kwa leo. Tukutane tena kesho.
Maoni